Masomo ya Misa
Dominika ya 20 ya Mwaka (Jumapili, Agosti 16, 2020)
Isa 56:1, 6-7
Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatenda haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.
Zab 67:1-2, 4-5, 7
Mungu na atufadhili na kutubariki,
na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
wokovu wake katikati ya mataifa yote.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
mataifa na washangilia,
naam, waimbe kwa furaha.
Maana kwa haki utawahukumu watu,
na kuwaongoza mataifa walioko duniani.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
watu na wakushukuru, Ee Mungu,
watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
miisho yote ya dunia itamcha Yeye.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Rum 11:13-15, 29-32
Nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa. Basi, naitukuza huduma iliyo yangu? Huenda nikapata kuwapatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao. Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa. Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake. Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao; kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema. Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.
Mdo 16:14
Aleluya, aleluya,
Fungua mioyo yetu, Ee Bwana,
Ili tuyatuze maneno ya Mwanao.
Aleluya
Mt 15:21-28
Yesu aliondoka huko, akaenda kando pande za tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.
Maoni
Leonard Dickson
Mwenyezi Mungu azidi kuwabariki katika kuifanya kazi yake izidi kuenea duniani kote.George Masaka
Amina.Ingia utoe maoni