Masomo ya Misa
Dominika ya 18 ya Mwaka (Jumapili, Agosti 02, 2020)
Isa 55:1-3
Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani. Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono. Tegeni masikio yenu, na kunijia; Sikieni, na nafsi zenu zitaishi; Nami nitafanya nanyi agano la milele, Naam, rehema za Daudi zilizo imara.
Zab 145:8-9, 15-18
Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.
Macho ya watu wote yakuelekea Wewe,
Nawe huwapa chakula chao wakati wake.
Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.
(K) Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.
Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu.
(K) Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.
Rum 8:35, 37-39
Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Yn 10:27
Aleluya, aleluya
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, asema Bwana; Nami nawajua, nao wanifuata
Aleluya
Mt 14:13-21
Yesu aliposikia hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto.
Maoni
Ingia utoe maoni