Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mt. Marta, Mlei (Jumatano, Julai 29, 2020)  

Somo la 1

Yer 15:10, 16–21

Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani. Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi. Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi; naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu. Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu? Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao. Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.

Wimbo wa Katikati

Zab 59:1–4, 9–10, 16–17

Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu,
Uniinue juu yao wanaoshindana nami.
Uniponye nao wafanyao maovu,
Uniokoe na watu wa damu.
(K) Bwana ulikuwa ngome yangu siku ya shida yangu.

Kwa maana wanaiotea nafsi yangu;
Wenye nguvu wamenikusanyikia;
Ee bwana, si kwa kosa langu,
Wala si kwa hatia yangu.
Bila kosa langu huenda mbio, hujiweka tawari;
Uamke uonane nami, na kutazama.
(K) Bwana ulikuwa ngome yangu siku ya shida yangu.

Ee nguvu zangu, nitakungoja Wewe,
Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu.
Mungu wa fadhili zangu atanitangulia,
Mungu atanijalia kuwatazama adui zangu.
(K) Bwana ulikuwa ngome yangu siku ya shida yangu.

Nami nitaziimba nguvu zako asubuhi,
Nitaziimba fadhili zako kwa furaha.
Kwa kuwa ndiwe uliyekuwa ngome yangu,
Na makimbilio siku ya shida yangu.
(K) Bwana ulikuwa ngome yangu siku ya shida yangu.

Ee nguvu zangu, nitakuimbia kwa furaha,
Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu,
Mungu wa fadhili zangu.
(K) Bwana ulikuwa ngome yangu siku ya shida yangu.

Shangilio

Yak 1:21

Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno la Mungu lililopandwa ndani liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.

Injili

Mt 13:44–46

Yesu aliwaambia makutano mifano, Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote akainunua.

Maoni


Ingia utoe maoni