Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 16 ya Mwaka (Jumapili, Julai 19, 2020)  

Somo la 1

Hek 12:13, 16-19

Hakuna Mungu mwingine ye yote ila Wewe, unayewaangalia watu wote, hata umwonyeshe huyo ya kuwa hukuhukumu bila haki. Madhali ndio uweza wako ulio asili ya haki, na kwa sabiki ya milki yako juu ya mambo yote unawaachilia wote. Kwa kuwa iwapo wanadamu hawasadiki ya kuwa umekamilika katika uweza wako, Wewe wazidhirisha nguvu zako; tena ukijishughulisha na wale wasioikiri kweli hiyo, waifadhaisha jeuri yao. Walakini desturi yako unauzuia hata uweza wako, na kuhukumu kwa upole, na kututawala kwa uvumilivu mwingi. Yaani uweza unao, wakati wo wote utakapo kuutumia. Pamoja na hayo, uliwafundisha watu wako kwa matendo yako ya namna hiyo ya kwamba imempasa mwenye haki kuwa mpenda wanadamu; tena ukawatilia wanao tumaini jema, kwa sababu, endapo watu wametenda dhambi, unawajalia toba.

Wimbo wa Katikati

Zab 86:5-6, 9-10, 15-16

Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe.
Na mwingi wa fadhili,
Kwa watu wote wakuitao.
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu.
(K) Kwa maana Wewe, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe.

Mataifa yote uliowafanya watakuja;
Watakusujudia Wewe, Bwana.
Watalitukuza jina lako;
Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu.
Wewe ndiwe mfanya miujiza,
Ndiwe Mungu peke yako.
(K) Kwa maana Wewe, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe.

Lakini Wewe, Bwana,
U Mungu wa rehema na neema.
Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli.
Unielekee na kunifadhili mimi.
(K) Kwa maana Wewe, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe.

Somo la 2

Rum 8:26-27

Roho hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.

Shangilio

Yn 17:17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli,
Ee Bwana, Ututakase sisi kwa ile kweli.
Aleluya.

Injili

Mt 13:24-43

Yesu aliwatolea mfano, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake. Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke. akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali. Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wa wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake; nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.

Maoni


Ingia utoe maoni