Masomo ya Misa
Jumanne ya 15 ya Mwaka (Jumanne, Julai 14, 2020)
Isa 7:1–9
Ilikuwa katika siku za Ahazi, mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, mfalme wa Yuda, Resini, mfalme wa Shamu, na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, wakapanda wakaenda Yerusalemu ili kupigana nao, lakini hawakuweza kuushinda. Kisha watu wa nyumba ya Daudi wakaambiwa kwamba Shamu wamefanya mapatano na Efraimu. Na moyo wake ukataharuki, na moyo wa watu wake, kama miti ya mwituni itikiswavyo na upepo. Basi Bwana akamwambia Isaya, Haya, toka, umlaki Ahazi, wewe na Shear-yashubu mwana wako, huko mwisho wa mfereji wa birika la juu, katika njia kuu ya uwanja wa dobi; ukamwambie, Angalia, ukatulie; usiogope wala usife moyo, kwa sababu ya mikia hii miwili ya vinga hivi vitokavyo moshi; kwa sababu ya hasira kali ya Resini na Shamu, na mwana wa Remalia. Kwa kuwa Shamu amekusudia mabaya juu yako, pamoja na Efraimu na mwana wa Remalia, wakisema, Haya, na tupande ili kupigana na Yuda na kuwasumbua, tukabomoe mahali tupate kuingia, na kummilikisha mfalme ndani yake, huyo mwana wa Tabeeli. Bwana MUNGU asema hivi, Neno hili halitasimama wala halitakuwa. Kwa maana kichwa cha Shamu ni Dameski, na kichwa cha Dameski ni Resini; na katika muda wa miaka sitini na mitano Efraimu atavunjika vipande vipande, asiwe kabila ya watu tena; tena kichwa cha Efraimu ni Samaria, na kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia. Kwamba hamtaki kusadiki, bila shaka hamtathibitika.
Zab 48:1–7
Bwana ndiye aliye mkuu,
Na mwenye kusifiwa sana.
Katika mji wa Mungu wetu,
Katika mlima wake mtakatifu.
Kuinuka kwake ni mzuri sana,
Ni furaha ya dunia yote.
(K) Mji wa mungu wetu ataufanya imara hata milele.
Mlima Sayuni pande za kaskazini,
Mji wa Mfalme mkuu.
Mungu katika majumba yake
Amejijulisha kuwa ngome.
(K) Mji wa mungu wetu ataufanya imara hata milele.
Maana, tazama, wafalme walikusanyika;
Walipita wote pamoja.
Waliona, mara wakashangaa;
Wakafadhaika na kukimbia.
(K) Mji wa mungu wetu ataufanya imara hata milele.
Papo hapo tetemeko liliwashika,
Utungu kama wa mwanamke azaaye.
Kwa upepo wa mashariki
Wavunja jahazi za Tarshishi.
(K) Mji wa mungu wetu ataufanya imara hata milele.
Zab 119:34
Aleluya, aleluya,
Unifahamishe name nitaishika sharia yako, nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya.
Mt 11:20–24
Yesu alianza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu. Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu. Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo. Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe.
Maoni
Ingia utoe maoni