Masomo ya Misa
Jumanne ya 14 ya Mwaka (Jumanne, Julai 07, 2020)
Hos 8:4–7, 11–13
Bwana asema hivi: Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali. Amemtupa ndama yako, Ee Samaria; hasira yangu imewaka juu yao; siku ngapi zitapita kabla ya hao kupata hali isiyo na hatia? Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjiaka vipande vipande. Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza. Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake. Nijapomwandikia sharia yangu katika amri elfu kumi, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni. Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini Bwana hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri.
Zab 115:3–10
Mungu wetu yuko mbinguni,
Alitakalo lote amelitenda.
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu.
(K) Enyi Israeli, mtumainini Bwana.
Zina vinywa lakini hazisemi,
Zina macho lakini hazioni,
Zina masikio lakini hazisikii,
Zina pua lakini hazisikii harufu.
(K) Enyi Israeli, mtumainini Bwana.
Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi,
Wala hazitoi sauti kwa koo zake.
Wazifanyao watafanana nazo,
Kila mmoja anayezitumainia.
(K) Enyi Israeli, mtumainini Bwana.
Enyi Israeli, mtumaini Bwana;
Yeye ni msaada wao na ngao yao;
Enyi mlango wa Haruni, mtumainini Bwana;
Yeye ni msaada wao na ngao yao.
(K) Enyi Israeli, mtumainini Bwana.
Efe 1:7, 18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
Mt 9:32–39
Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wowote. Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo. Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na laipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apelike watenda kazi katika mavuno yake.
Maoni
Ingia utoe maoni