Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 12 ya Mwaka (Jumatatu, Juni 22, 2020)  

Somo la 1

2Fal 17:5–8, 13–15, 18

Mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu. Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya Bwana, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya. Pamoja na hayo Bwana aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu. Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa nguvu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini Bwana, Mungu wao. Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao Bwana alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao. Kwa hiyo Bwana akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake.

Wimbo wa Katikati

Zab 60:1–3, 10–11

Ee Mungu, umetutupa na kututawanya,
Umekuwa na hasira, uturudishe tena.
(K) Uokoe kwa mkono wako wa kuume, Ee Bwana, utuitikie.

Umeitetemesha nchi na kuipasua,
Upaponye palipobomoka, maana inatikisika.
Umewaonyesha watu wako mazito,
Na kutunywesha mvinyo ya kutuyumbisha.
(K) Uokoe kwa mkono wako wa kuume, Ee Bwana, utuitikie.

Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa?
Wala, Ee Mungu, hutoki na majeshi yetu?
Utuletee msaada juu ya mtesi,
Maana wokovu wa binadamu haufai.
(K) Uokoe kwa mkono wako wa kuume, Ee Bwana, utuitikie.

Shangilio

Zab 119:28, 33

Aleluya, aleluya,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako, ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya.

Injili

Mk 7:1–5

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msihukumu msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.

Maoni


Ingia utoe maoni