Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Mt. Antoni wa Padua, Padre na Mwalim (Jumamosi, Juni 13, 2020)
1Fal 19:19-21
Eliya aliondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng’ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng’ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda urudi; ni nini niliyokutendea. Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng’ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng’ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.
Zab 16:1-2, 5, 7-10
Mungu, unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Sina wema ila utokao kwako.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu.
Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu.
Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Na utukufu wangu unashangilia,
Naam mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu,
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu.
Yak 1:21
Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno la Mungu lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.
Mt 5:33-37
Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa: Usizini, ila mtimizie Bwana nyapo zako; lakni mimi nawaambia: Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.
Maoni
Ingia utoe maoni