Masomo ya Misa
Dominika ya 6 ya Pasaka (Jumapili, Mei 17, 2020)
Mdo 8:5-8, 14-17
Filipo alitelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.
Zab 66:1-7, 16, 20
Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake, Tukuzeni sifa zake.
Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini!
(K) Mpigieni Mungu kelele za shangwe nchi yote
Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu;
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu;
(K) Mpigieni Mungu kelele za shangwe nchi yote
Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko mlikomfurahia.
Atawala kwa uweza wake milele;
(K) Mpigieni Mungu kelele za shangwe nchi yote
Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu,
Wala kuniondolea fadhili zake.
(K) Mpigieni Mungu kelele za shangwe nchi yote
1Pet 3:15-18
Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,
Yn 14:23
Aleluya, aleluya
Yesu alisema: Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake.
Aleluya
Yn 14:15-21
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.
Maoni
Ingia utoe maoni