Masomo ya Misa
Jumanne ya 4 ya Pasaka (Jumanne, Mei 05, 2020)
Mdo 11:19-26
Siku zile, wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.
Zab 87:1-7
Msingi wake upo Juu ya milima mitakatifu.
Bwana ayapenda malango ya Sayuni Kuliko maskani zote za Yakobo.
Umetajwa kwa mambo matukufu, Ee Mji wa Mungu.
(K) Enyi mataifa yote msifuni Bwana.
Nitataja Rahabu na Babeli Miongoni mwao wanaonijua.
Tazama Filisti, na Tiro, na Kushi; Huyu alizaliwa humo.
Naam, mintarafu Sayuni itasemwa,
Huyu na huyu alizaliwa humo.
Na Yeye Aliye juu Ataufanya imara.
(K) Enyi mataifa yote msifuni Bwana.
Bwana atahesabu, awaandikapo mataifa,
Huyu alizaliwa humo.
Waimbao na wachezao na waseme,
Visima vyangu vyote vimo mwako.
(K) Enyi mataifa yote msifuni Bwana.
Yn 10:22-30
Huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi. Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani. Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi. Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia. Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu. Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.
Maoni
Ingia utoe maoni