Masomo ya Misa
Dominika ya 13 ya Mwaka (Jumapili, Juni 26, 2016)
1 Fal 19:16b, 19-21
Bwana alimwambia Eliya: Enenda, mtie mafuta Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako. Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng'ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea? Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng'ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng'ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.
Zab 16:1-2, 5, 7-11
Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; Sina wema ila utokao kwako.
(K)Bwana ndiye fungu la posho langu.
Bwana ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
(K)Bwana ndiye fungu la posho langu.
Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, Naam,
mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
(K)Bwana ndiye fungu la posho langu.
Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu,
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.
(K)Bwana ndiye fungu la posho langu.
Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.
(K)Bwana ndiye fungu la posho langu.
Gal 5:1,13-18
Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako. Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana. Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.
Yn 17:7
Aleluya, aleluya
Neno lako ndiyo kweli, ee Bwana; Ututakase sisi kwa ile kweli
Aleyuya
Lk 9:51-62
Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu; akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]? Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.] Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine. Nao walipokuwa wakienda njiani, mtu mmoja alimwambia, Nitakufuata ko kote utakakokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu. Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu. Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.
Maoni
Ingia utoe maoni