Masomo ya Misa
Ijumaa ya 2 ya Pasaka (Ijumaa, Aprili 24, 2020)
Mdo 5:34-42
Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu. Wakakubali maneno yake; nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo. Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.
Zab 27:1, 4, 13-14
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K)Neno moja nimelitaka kwa Bwana, Nikae nyumbani mwa Bwana.
Neno Moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake.
(K)Neno moja nimelitaka kwa Bwana, Nikae nyumbani mwa Bwana.
Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
(K)Neno moja nimelitaka kwa Bwana, Nikae nyumbani mwa Bwana.
Kol 3:1
Aleluya, aleluya.
Mkiwa mmefufuliwa na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
Yn 6:1-15
Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu. Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni. Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.
Maoni
Ingia utoe maoni