Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 2 ya Pasaka (Jumapili, Aprili 19, 2020)  

Somo la 1

Mdo 2:42–47

Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume. Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, walimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.

Wimbo wa Katikati

Zab 11:2–4, 13–15, 22–24

Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Mlango wa Haruni na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.

Ulinisukuma sana ili nianguke;
Lakini Bwana akanisaidia.
Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu,
Naye amekuwa wokovu wangu.
Sauti ya furaha na wokovu
Imo hemani mwao wenye haki.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.

Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu.
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
Tutaishangilia na kuifurahia.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.

Somo la 2

1Pet 1:3–9

Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya Imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho. Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa Imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufufunuliwa kwake Yesu Kristo. Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu, katika kuupokea mwisho wa Imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu.

Shangilio

Yn 20:29

Aleluya, aleluya,
Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadfiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.

Injili

Yn 20:19–31

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini na uzima kwa jina lake.

Maoni


Ingia utoe maoni