Masomo ya Misa
Alhamisi ya 4 ya Kwaresima (Alhamisi, Machi 26, 2020)
Kut 32:7-14
Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia kuyeyusha, wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu; basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami ninakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ilia pate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu, nao watairithi milele. Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.
Zab 106:19-23
Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
Wakaubadili utukufu wao
Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani.
(K) Ee Bwana unikumbuke mimi, kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri.
(K) Ee Bwana unikumbuke mimi, kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
Akasema ya kuwa atawaangamiza,
Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,
Mbele zake kama mahali palipobomoka,
Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.
(K) Ee Bwana unikumbuke mimi, kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
Mt 4:17
Tubuni, asema Bwana, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
Yn 5:31-47
Yesu aliwambia Wayahudi: Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayeshuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohane, naye akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda. Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohane; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye. Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo. Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?
Maoni
Ingia utoe maoni