Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 2 ya Kwaresima (Ijumaa, Machi 13, 2020)  

Somo la 1

Mwa 37:3-4, 12-13, 17-28

Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, na hawakuweza kusema naye kwa amani. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shuri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula. Wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanyabiashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

Wimbo wa Katikati

Zab 105:16-21

Akaiita njaa iijilie nchi,
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu utumwani.
(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.

Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu.
(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.

Mfalme alituma watu akamfungua,
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote.
(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.

Shangilio

Yn 3:16

Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.

Injili

Mt 21:33-43; 45-46

Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Ataangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, linguine lenye kuzaa matunda yake. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

Maoni


Ingia utoe maoni