Masomo ya Misa
Jumatatu ya 1 ya Kwaresima (Jumatatu, Machi 02, 2020)
Law 19:1-2, 11-18
Bwana akanena na Musa, akamwambia, Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu. Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo. Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi. Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; Mimi ndimi Bwana. Usimchukie ndigu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako nafsi yako; Mimi ndimi Bwana.
Zab 19:7-9, 14
Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.
(K) Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.
Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru.
(K) Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.
Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele,
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa.
(K) Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.
Maneno ya kinywa changu,
Na mawazo ya moyo wangu,
Yapate kibali mbele zake, Ee Bwana,
Mwamba wangu, na mwokozi wangu.
(K) Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.
Zab 51:1-10, 12
Ee Mungu, uniumbie mioyo yenu; Unirudishie furaha ya wokovu wako.
Mt 25:31-46
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kodnoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme, mliowekewa tayari tangu kuubwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
Maoni
Ingia utoe maoni