Masomo ya Misa
Ijumaa baada ya Majivu (Ijumaa, Februari 28, 2020)
Isa 58:1-9
Bwana Mungu asema hivi: Piga kelele, usiache paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao, na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wakinitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uvou. Hamfungi siku hii ya leo hata kuiskizisha sauti yenu juu. Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Si siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana. Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya ayko itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na Bwana ataitika; atalia, naye atasema, Mimi hapa.
Zab 51:3-4, 5-6a, 18-19
Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu I mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako.
Na kufanya maovu mbele za macho yako.
(K) Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutadharau.
Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni;
Nawe utanijulisha hekima kwa siri.
(K) Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutadharau.
Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
Uzijenge kuta za Yerusalemu.
Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki;
Na sadaka za kuteketezwa, na kafara.
(K) Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutadharau.
Eze 18:31
Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; Jifanyieni moyo mpya na roho mpya.
Mt 9:14-15
Siku ile: Yesu alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, wanafunzi wake Yohane wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.
Maoni
Ingia utoe maoni