Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 6 ya Mwaka (Jumatano, Februari 19, 2020)  

Somo la 1

Yak 1:19-27

Ndugu zangu wapenzi, mnajua kwamba kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu. Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.

Wimbo wa Katikati

Zab 15:1-5

Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako?
Ni nani atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, Na kutenda haki.
Asemaye kweli kwa moyo wake,
(K) Ni nani atakayefanya maskani yake katika kilima chako kitakatifu, Ee Bwana?

Asiyesingizia kwa ulimi wake.
Wala hakumtenda mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao
(K) Ni nani atakayefanya maskani yake katika kilima chako kitakatifu, Ee Bwana?

Hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.
(K) Ni nani atakayefanya maskani yake katika kilima chako kitakatifu, Ee Bwana?

Injili

Mk 8:22-26

Wakati ule, Yesu na wanafunzi wake walifika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse. Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu? Akatazama juu, akasema, Naona watu kama miti, inakwenda. Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi. Akampeleka nyumbani kwake, akisema, Hata kijijini usiingie.

Maoni


Ingia utoe maoni