Masomo ya Misa
Jumatano ya 5 ya Mwaka (Jumatano, Februari 12, 2020)
1Fal 10:1-10
Malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hakima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa naye, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amkufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki. Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani.
Zab 37:5-6, 30-31, 39-40
Umkabidhi Bwana njia yako,
Pia umtumaini naye atafanya.
Akaitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri.
(K) Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.
Kinywa cha mwenye haki hunena hekima,
Na ulimi wake husema hukumu.
Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake,
Hatua zake hazitelezi.
(K) Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.
Wokovu wa wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
Huwaopoa wasio haki na kuwaokoa,
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.
(K) Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.
Yn 17:17
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, neno lako ndiyo kweli, uwatakase kwa hiyo kweli.
Aleluya.
Mk 7:14–23
Yesu aliwaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.
Maoni
Ingia utoe maoni