Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 4 ya Mwaka (Ijumaa, Februari 07, 2020)  

Somo la 1

Ybs 47:2-11

Kama mafuta yalivyotengwa na kafara ya amani, vivyo hivyo Daudi alitengwa na wana wa Israeli. Naye alicheza pamoja na simba kana kwamba ni wana-mbuzi, pia pamoja na dubu kana kwamba ni wana-kondoo wa kundi. Je! Hakumwua jitu katika ujana wake, akawaondolea watu lawama; alipouinua mkono wake na jiwe la teo, akayashusha majivuno ya Goliathi? Kwa maana alimwita Aliye juu; na yeye akaitia nguvu yamini yake; ili amwue shujaa hodari wa vita; ili aiinue pembe ya watu wake. Kwa hiyo binti za watu wakamtukuza wakiimbiana, na kumheshimu alivyoua makumi elfu yake; naye alipokwisha kuivaa taji ya utukufu, alipigana na adui na kuwashinda pande zote; akajenga maboma yake kati ya Wafilisti, akaivunja pembe yao vipande vipande, hata siku hii ya leo. Katika kila kazi yake Daudi alimshukuru Mungu Aliye juu kwa maneno matukufu; na kwa moyo wake wote akampenda Muumba wake, akamhimidi kila siku daima. Pia akaweka waimbaji mbele ya madhabahu, ili watoe sauti tamu katika kuimba kwao. Akauongeza uzuri wa sikukuu, akaziratibisha nyakati katika ukamilifu; pindi walipolihimidi jina takatifu la Bwana hata patakatifu pakavuma sauti tokea asubuhi na mapema. Naye Bwana akamwondolea dhambi zake, akiinua pembe yake hata milele; akampa agano la ufalme, na kiti kitakatifu cha enzi katika Israeli.

Wimbo wa Katikati

Zab 18:30, 46, 49-50

Mungu, njia yake ni kamilifu,
Ahadi ya Bwana imehakikishwa,
Yeye ndiye ngao yao. Wote wanaomkimbilia.
(K) Atukuzwe Mungu wa wokovu wangu.

Bwana ndiye aliye hai;
Na ahimidiwe mwamba wangu;
Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu;
Basi, Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa,
Nami nitaliimbia jina lako.
(K) Atukuzwe Mungu wa wokovu wangu.

Ampa mfalme wake wokovu mkuu,
Amfanyia fadhili masihi wake,
Daudi na mzao wake hata milele.
(K) Atukuzwe Mungu wa wokovu wangu.

Injili

Mk 6:14-29

Mfalme Herode alisikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

Maoni


Ingia utoe maoni