Masomo ya Misa
Jumamosi ya 11 ya Mwaka (Jumamosi, Juni 18, 2016)
2 Nya 24:17-25
Baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao. Wakaiacha nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao. Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa Bwana; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza. Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi. Basi, wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya Bwana. Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, Bwana na ayaangalie haya, akayatakie kisasi. Ikawa mwisho wa mwaka, wakakwea juu yake jeshi la Washami; wakafika Yuda na Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wa watu wote miongoni mwa watu, wakamletea mfalme wa Dameski nyara zao zote. Maana wakaja jeshi la Washami watu haba; Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa mno, kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao. Hivyo wakamfanyia Yoashi hukumu. Hata walipoondoka kwake, (nao walimwacha ameshikwa sana na maradhi,) watumishi wake mwenyewe wakamfanyia fitina kwa ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada kuhani, wakamwua kitandani pake, akafa; wakamzika mjini mwa Daudi, lakini hawakumzika katika makaburi ya wafalme.
Zab 89:3-4, 28-33
Nimefanya agano na mteule wangu, Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele, Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele.
(K)Nitamwekea fadhili zangu milele.
Hata milele nitamwekea fadhili zangu, Na agano langu litafanyika amini kwake.
Wazao wake nao nitawadumisha milele, Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.
(K)Nitamwekea fadhili zangu milele.
Wanawe wakiiacha sheria yangu, Wasiende katika hukumu zangu,
Wakizihalifu amri zangu, Wasiyashike maagizo yangu,
(K)Nitamwekea fadhili zangu milele.
Basi, nitawarudi makosa yao kwa fimbo, Na uovu wao kwa mapigo.
Lakini fadhili zangu sitamwondolea yeye, Wala sitafanya uaminifu wangu kuwa uongo.
(K)Nitamwekea fadhili zangu milele.
2 Kor 8:9
Aleluya, aleluya
Bwana wetu Yesu Kristo alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.
Aleluya
Mt 6:24-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake;Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni