Alhamisi. 28 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mt. Agata, Bikira na Shahidi (Jumatano, Februari 05, 2020)  

Somo la 1

2Sam 24:2, 9-17

Mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu. Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu. Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema, Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. Basi Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, Bwana akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa Bwana alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na Bwana, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu.

Wimbo wa Katikati

Zab 32:1-2, 5-7

Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makosa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
Ambaye rohoni mwake hamna hila.
(K) Ee Bwana, unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.
(K) Ee Bwana, unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Kwa hiyo kila mtu mtauwa Akuombe wakati unapopatikana.
Hakika maji makuu yafurikapo, Hayatamfikia yeye.
(K) Ee Bwana, unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,
Utanizungusha nyimbo za wokovu.
(K) Ee Bwana, unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Injili

Mk 6:1-6

Yesu alitoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Maoni


Ingia utoe maoni