Alhamisi. 28 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 4 ya Mwaka (Jumatatu, Februari 03, 2020)  

Somo la 1

2Sam 15:13-14, 30, 16:5-13

Mjumbe alimfikia Daudi, akasema, Mioyo ya watu wa Israeli inashikamana na Absalomu. Basi Daudi akawaambia watumishi wake wote waliokuwa pamoja naye Yerusalemu, Ondokeni, tukakimbie; kwa kuwa tusipokimbia hapana mtu miongoni mwenu atakayeokoka mikononi mwa Absalomu; haya! Fanyeni haraka, tuondoke, asitupate kwa upesi, na kutuletea maovu, na kuupiga mji huu kwa makali ya upanga. Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake; akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda. Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli, ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu. Ndipo Abishai, mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi; basi, ni nani atakayesema, Mona umetenda haya? Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si Zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza. Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo. Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake.

Wimbo wa Katikati

Zab 3:1-7

Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi,
Ni wengi wanaonishambulia,
Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu:
Hana wokovu huyu kwa Mungu.
(K) Bwana, uinuke, uniokoe.

Na Wewe, Bwana, u ngao yangu pande zote,
Utukufu wangu namwinua kichwa changu.
Kwa sauti yangu namwita Bwana,
Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu.
(K) Bwana, uinuke, uniokoe.

Nalijilaza nikalala usingizi,
Nikaamka kwa kuwa Bwana ananitegemeza.
Sitayaogopa makumi elfu ya watu
Waliojipanga juu yangu pande zote.
Bwana, uinuke, Mungu wangu, uniokoe.
(K) Bwana, uinuke, uniokoe.

Shangilio

Lk 7:16

Aleluya, aleluya,
Nabii mkuu ametokea kwetu, Mungu amewaangalia watu wake.
Aleluya.

Injili

Mk 5:1–20

Yesu na wanafunzi wake walifika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa pale makaburini; wal ahakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakatia kwa mawe. Na laipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile. Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha. Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini. Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashamba. Watu wakatoka walione lililotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, ndiye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe. Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao. Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu. Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.

Maoni


Ingia utoe maoni