Masomo ya Misa
Jumanne ya 4 ya Majilio (Jumanne, Desemba 24, 2019)
2Sam 7:1-5, 8-11, 16
Ikawa, mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa nyumba mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Nalikutwa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena Bwana anakuambia ya kwamba Bwana atakujengea nyumba. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.
Zab 89:1-4, 27, 29
Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa change nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
(K) Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele;
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele.
(K) Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza;
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
Wazao wake nao nitawadumisha milele,
Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.
(K) Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
Shangilio
Aleuya, aleluya,
Ee Utokaye Mashariki, Uliye mnga’ao wa mwanga wa milele na jua la haki, Njoo kuwaangazia wakaao gizani na katika kivuli cha mauti.
Aleluya.
Lk 1:67-79
Siku ile, Zakaria, baba yake Yohane alijazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema, Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo kwa kinywa cha manabii wake watakatifu; tuokolewe na adui zetu na mikononi mwao wote wanaotuchukia; ili kuwatendea rehema baba zetu, na kulikumbuka agano lake takatifu; uapo aliomwambpia Ibrahimu, baba yetu, ya kwamba atatujalia sisi, tuokoke mikononi mwa adui zetu, na kumwabudu pasipo hofu, kwa utakatifu na kwa haki mbele zake siku zetu zote. Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake aliye juu, kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umemtengenezea njia zake; uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya Amani.
Maoni
Ingia utoe maoni