Masomo ya Misa
Jumatatu ya 11 ya Mwaka (Jumatatu, Juni 13, 2016)
1 Fal 21:1-16
Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki.
Zab 5:2-3, 5-7
Uisikie sauti ya kilio changu, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu,
Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye.
Bwana, asubuhi utaisikia sauti yangu,
Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia.
(K)Uisikie sauti ya kilio changu, ee Bwana.
Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako;
Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
(K)Uisikie sauti ya kilio changu, ee Bwana.
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila
Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako,
Nitaingia nyumbani mwako; Na kusujudu kwa kicho,
Nikilielekea hekalu lako takatifu.
(K)Uisikie sauti ya kilio changu, ee Bwana.
Zab 119:105
Aleluya, aleluya
Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
Aleluya
Mt 5:38-42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.
Maoni
Ingia utoe maoni