Masomo ya Misa
Jumatano ya 2 ya Majilio (Jumatano, Desemba 11, 2019)
Isa 40:25-31
Mtanifananisha na nani, nipate kuwa sasa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake. Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie? Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Haya vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.
Zab 103:1-4, 8, 10
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Naam, vyote vilivyo ndani yangu,
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema.
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hakututenda sawasawa na hatia zetu.
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana atakuja kuwaokoa watu wake, Heri walio tayari kumlaki.
Aleluya.
Mt 11:28-30
Siku ile, Yesu alijibu akasema: Njoni kwangu nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
Maoni
Ingia utoe maoni