Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 11 ya mwaka (Jumapili, Juni 12, 2016)  

Somo la 1

2 Sam 12:7-10, 13

Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha. Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.

Wimbo wa Katikati

Zab 32:1-2, 5, 7, 11




Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.
((K) Unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Nalikujulisha dhambi yangu, Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.
((K) Unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,
Utanizungusha nyimbo za wokovu.
((K) Unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Mfurahieni Bwana; Shangilieni,
enyi wenye haki Pigeni vigelegele vya furaha;
Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo.
((K) Unisamehe upotovu wa dhambi yangu.

Somo la 2

Gal 2:16, 19-21

Hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki. Maana mimi kwa njia ya sheria naliifia sheria ili nimwishie Mungu. Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu. Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure.

Shangilio

Yn 8:12

Aleluya, aleluya
Mimi ndimi Nuru ya ulimwengu, asema Bwana; yeye amfuataye hatakwenda gizani kamwe.
Aleluya

Injili

Lk 7:36—8:3

Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake yule Farisayo, akaketi chakulani. Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu. Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena. Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki. Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake. Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo. Kisha alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako. Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi? Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani.Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.

Maoni


Ingia utoe maoni