Masomo ya Misa
Jumamosi ya 10 ya Mwaka, Mt. Barnaba Mtume (Jumamosi, Juni 11, 2016)
Mdo 11:21-26, 13:1-3
Watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.
Zab 98:1-6
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K)Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa
Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K)Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa
Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K)Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
(K)Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa
Zab 119:36a, 29b
Aleluya , aleluya
Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako,Unineemeshe kwa sheria yako.
Aleluya
Mt 10:7-13
Yesu aliwaambia mitume wake, katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.
Maoni
Ingia utoe maoni