Masomo ya Misa
Jumanne ya 34 ya Mwaka (Jumanne, Novemba 26, 2019)
Dan 2:31-45
Danieli alimwambia Nebukadreza: Wewe, Ee mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, ilivyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha. Na sanamu hii, kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi, kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba; miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo. Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. Ndipo kile chuma, na ule udongo na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja, vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha, hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa mlima mkubwa, likaijaza dunia yote. Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme. Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu; na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe, u kichwa kile cha dhahabu. Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote. Na ufalme wan ne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunjavunja na kuseta. Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope. Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika. Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo. Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. Na kama vile ulivyoona ya kuwa jiwe lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunjwavunjwa kile chuma, na ile shaba, na ule udongo, na ile fedha, na ile dhahabu; basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti.
Dan 3:57-61
Enyi viumbe vyote vya Bwana mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni Bwana na kumwadhimisha milele.
Enyi mbingu, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni Bwana na kumwadhimisha milele.
Yak 1:18
Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenye, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.
Lk 21:5-11
Watu wa kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, Yesu alisema, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.
Maoni
Ingia utoe maoni