Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Mtakatifu Martino wa Tours, Askofu (Jumatatu, Novemba 11, 2019)
Hek 1:1-7
Pendeni haki, enyi waamuzi wa dunia; Tafakarini habari za Bwana kwa moyo mwema. Na kumtafuta katika unyofu wa moyo. Kwa sababu huonekana nao wasiomjaribu, na kufunuliwa kwao wasiokosa kumwamini. Mradi fikira zilizopotoka hutenga wanadamu na Mungu, na enzi yake ikijaribiwa, huwafadhaisha wajinga. Hekima haiingii katika roho ya mtu awazaye maovu, wala haikai katika mwili wa mtu aliyefungwa rehani na dhambi. Kwa kuwa roho takatifu yenye maadili huikimbia hila, hubumburuka kujiepusha na fikira zisizo na akili, hufadhaika kuingiwa na udhalimu. Maana Hekima ni roho ambayo huwapenda wanadamu, wala haimwachilii mkufuru hatia ya midomo yake; kwa sababu Mungu huvishuhudia viuno vyake, na kuusimamia hasa moyo wake, na kuusikiliza ulimi wake. Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inayoviungamanisha viumbe vyote hujua maana ya kila sauti.
Zab 139:1-10
Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Uniongoze katika njia ya milele, Ee Bwana.
Maana hamna neno ulimini mwangu
Usilolijua kabisa, Bwana.
Umenizingira nyuma na mbele,
Ukaniwekea mkono wako.
Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi,
Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.
(K) Uniongoze katika njia ya milele, Ee Bwana.
Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko,
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
(K) Uniongoze katika njia ya milele, Ee Bwana.
Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika.
(K) Uniongoze katika njia ya milele, Ee Bwana.
2Kor 5:19
Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristu, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.
Lk 17:1–6
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusaga lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kulikko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni. Kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe. Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee Imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na Imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka ukapandwe baharini, nao ungewatii.
Maoni
Ingia utoe maoni