Masomo ya Misa
Alhamisi ya 29 ya Mwaka (Alhamisi, Oktoba 24, 2019)
Rum 6:19-23
Nasema kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa. Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na haki. Ni faida gani basi mliyopata siku zile kwa mambo hayo mnayoyatahayarikia sasa? Kwa maana mwisho wa mambo hayo ni mauti. Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele. Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Zab 1:1-4, 6
Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake
Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.
(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake
Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea.
(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake
Lk 12:49-53
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe! Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.
Maoni
Ingia utoe maoni