Jumamosi. 03 Mei. 2025

Masomo ya Misa

Watakatifu Malaika Walinzi (Jumatano, Oktoba 02, 2019)  

Somo la 1

Kut 23:20-23

Bwana asema hivi: Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali.

Wimbo wa Katikati

Zab 91:1-6, 10-11

Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu nitakayemtumaini.
(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.

Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji,
Na katika tauni iharibuyo.
Kwa manyoya yake atakufunika,
Chini ya mbawa zake utapata kimbilio;
Uaminifu wake ni ngao na kigao.
(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.

Hutaogopa hofu ya usiku,
Wala mshale urukao mchana,
Wala tauni ipitayo gizani,
Wala uele uharibuo adhuhuri,
(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.

Mabaya hayatakupata wewe,
Wala tauni haitaikaribia hema yako.
Kwa kuwa atakuagizia malaika zake
Wakulinde katika njia zako zote.
(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.

Injili

Mt 18:1-5, 10

Wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi; bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari. Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni

Title

Text