Masomo ya Misa
Jumatatu ya 26 ya Mwaka (Jumatatu, Septemba 30, 2019)
Zek 8:1-8
Neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema, Bwana wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu. Bwana asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa Bwana wa majeshi utaitwa, Mlima mtakatifu. Bwana wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana. Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake. Bwana wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je! Liwe neno gumu mbele ya macho yangu? Asema Bwana wa majeshi. Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi; nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.
Zab 102:15-20, 28, 21-22
Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
Atakapoonekana katika utukufu wake,
Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
Asiyadharau maombi yao.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.
Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,
Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
Na kuwafungua walioandikiwa kufa.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.
Wana wa watumishi wako watakaa,
Na wazao wao wataimarishwa mbele zako.
Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni,
Na sifa zake katika Yerusalemu,
Pindi mataifa watapokusanyika pamoja,
Falme nazo ili kumtumikia Bwana.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.
Lk 9:46-50
Wanafunzi waliaanza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao. Naye Yesu alipotambua mawazo ya mioyo yao, alitwaa mtoto mdogo akamweka karibu naye, akawaambia, Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa. Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu.
Maoni
Ingia utoe maoni