Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 26 ya Mwaka (Jumapili, Septemba 29, 2019)  

Somo la 1

Amo 6:1,4-7

Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya masemadari yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini; ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi; ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu. Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za machezo za hao waliojinyosha zitakoma.

Wimbo wa Katikati

Zab 146:6-10

Huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa;
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana

Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni;
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana

Huwategemeza yatima na mjane;
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana

Somo la 2

1Tim 6:11-16

Wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole. Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi. Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato, kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana; ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.

Shangilio

Yn 17:17

Aleluya, aleluya
Neno lako ndiyo kweli, ee Bwana; Ututakase sisi kwa ile kweli.
Aleluya

Injili

Lk 16:19-31

Yesu aliwaambia Mafarisayo, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.

Maoni


Ingia utoe maoni