Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 10 ya Kwaka (Jumapili, Juni 05, 2016)  

Somo la 1

1 Fal 17:17-24

Mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu? Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la Bwana kinywani mwako ni kweli.

Wimbo wa Katikati

Zab 30:1, 3-5,10-12

Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
(K) Ee Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua

Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao shimoni.
(K) Ee Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua

Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani.
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.
(K) Ee Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua

Ee Bwana, usikie, unirehemu, Bwana, uwe msaidizi wangu.
(K) Ee Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua

Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
(K) Ee Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua

Ili utukufu wangu ukusifu, Wala usinyamaze. Ee Bwana, Mungu wangu, Nitakushukuru milele.
(K) Ee Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua

Somo la 2

Gal 1:11-19

Ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana.

Shangilio

1Sam 3:9; Yn 6:8

Aleluya, aleluya
Nena Bwana kwa maana mtumishi wako anasikia; wewe unayo maneno ya uzima wa milele
Aleluya

Injili

Lk 7:11-17

Yesu alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.

Maoni


Ingia utoe maoni