Masomo ya Misa
Jumamosi ya 25 ya Mwaka (Jumamosi, Septemba 28, 2019)
Zek 2:1-5, 10-11
Niliinua macho yangu, nikaona, na tazama, mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake. Ndipo nikasema, unakwenda wapi? Akaniambia, Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione upana wake ulivyo na urefu wake ulivyo. Na tazama, yule malaika aliyesema nami akasimama karibu, na malaika mwingine akatoka ili kuonana naye; naye akamwambia, Piga mbio, kamwambie kijana huyu, na kusema, Yerusalemu utakaliwa na watu, kama vijiji visivyo na kuta, kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo ndani yake. Kwa maana mimi, asema Bwana, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakaa, kati yako, asema Bwana. Na mataifa mengi watajiunga na Bwana katika siku ile, nao watakuwa watu wangu.
Yer 31:10-13
Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa,
Litangazeni visiwani mbali, mkaseme,
Aliyemtawanya Israeli atamkusanya,
Na kumlinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
Amemkomboa mkononi mwake
aliyekuwa hodari kuliko yeye.
(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni,
wataukimbilia wema wa Bwana,
nafaka, na divai, na mafuta,
na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe.
Na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji,
Wala hawatahuzunika tena kabisa.
(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
Na vijana na wazee pamoja.
Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
Nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.
(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
Zab 119:18
Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.
Lk 9:43–45
Makutano walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.
Maoni
Ingia utoe maoni