Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Mt. Visenti wa Paulo (Padri) (Ijumaa, Septemba 27, 2019)
Hag 1:1, 2:2-9
Katika mwaka wa pili wa Dario mfalme, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake Hagai nabii, kusema, Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hayo mabaki ya watu, ukisema, Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu? Lakini sasa uwe hodari, Ee Zerubabeli, asema Bwana; nawe uwe hodari, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni hodari, enyi watu wote wa nchi hii, asema Bwana; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema Bwana wa majeshi; kama neno lile nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope. Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu; nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema Bwana wa majeshi. Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi. Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema Bwana wa majeshi.
Zab 43:1-4
Ee Bwana, unihukumu,
unitetee kwa taifa lisilo haki,
Uniokoe na mtu wa hila asiye haki.
(K) Umtumaini Mungu, kwa maana nitakuja kumsifu aliye afya ya uso wangu na Mungu wangu
Kwa kuwa Wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu;
kwa nini umenitupa?
Kwa nini ninakwenda nikihuzunika,
adui wakinionea?
(K) Umtumaini Mungu, kwa maana nitakuja kumsifu aliye afya ya uso wangu na Mungu wangu
Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako.
(K) Umtumaini Mungu, kwa maana nitakuja kumsifu aliye afya ya uso wangu na Mungu wangu
Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,
kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu;
Nitakusifu kwa kinubi,
Ee MUNGU, Mungu wangu.
(K) Umtumaini Mungu, kwa maana nitakuja kumsifu aliye afya ya uso wangu na Mungu wangu
Lk 9:18-22
Yesu alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? Wakamjibu wakisema, Yohana Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu. Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo; akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.
Maoni
Ingia utoe maoni