Masomo ya Misa
Jumanne ya 25 ya Mwaka (Jumanne, Septemba 24, 2019)
Ezr 6:7-8, 12, 14-20
Mfalme Dario alimwandikia liwali wa ng’ambo wa mto, na wenzake; Waacheni liwali wa Wayahudi na wazee wa Wayahudi, waijenge nyumba hii ya Mungu mahali pake. Tena, natoa amri kuwaagiza ninyi mtakayowatendea wazee hao wa Wayahudi kwa kazi hii ya kuijenga nyumba ya Mungu; katika mali ya mfalme, yaani, katika kodi za nchi iliyo ng’ambo ya Mto, watu hao wapewe gharama zote kwa bidii, ili wasizuiliwe. Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na aangamize wafalme wote, na watu wote, watakonyosha mikono yao kulibadili neno hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Mimi, Dario, nimetoa amri; na ifanyike kwa bidii nyingi. Nao wazee wa Wayahudi wakajenga, wakafanikiwa, kwa masaada wa kuhubiri kwao Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido. Wakajenga, wakaimaliza kazi yao, kwa maagizo ya Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi, na Dario, na Artashasta mfalme wa Uajemi. Nyumba hiyo ikamalizika siku ya tatu ya mwezi Adari, katika mwaka wa sita wa kutawala kwake mfalme Dario. Na wana wa Israeli, na makuhani, na walawi na watu wengine katika hao waliohamishwa, wakaiweka wakfru nyumba ya Mungu kwa furaha. Na katika kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, wakatoa sadaka, ng’ombe mia, na kondoo waume mia mbili, na wanakondoo mia nne; tena wakatoa mbuzi waume kumi na wawili, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli wote, kwa hesabu ya kabila za Israeli. Wakawaweka makuhani katika kura zao, wakawaweka na Walawi vilivyoandikwa katika chuo cha Musa. Kisha, wana wa uhamisho wakaifanya Pasaka, mwezi wa kwanza, siku ya kumi nan ne ya mwezi. Kwa maana makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa wote pamoja; wote walikuwa hali ya tohara; wakachinja pasaka kwa ajili ya wana wote wa uhamisho, na kwa ajili ya ndugu zao makuhani, na kwa ajili ya nafsi zao.
Zab 122:1-5
Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, ee Yerusalemu!
Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana.
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana;
Ushuhuda wa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi.
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.
1Pet 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
Lk 8:19–21
Walimwendea Yesu mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. Akaletewa habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe. Akawajibu akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
Maoni
Ingia utoe maoni