Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jina Takatifu la Maria (Alhamisi, Septemba 12, 2019)  

Somo la 1

Kol 3:12-17

Kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.

Wimbo wa Katikati

Zab 150:1-6

Msifuni Mungu katika patakatifu pake;
Msifuni katika anga la uweza wake.
Msifuni kwa matendo yake makuu;
Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
(K) Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana.

Msifuni kwa mvumo wa baragumu;
Msifuni kwa kinanda na kinubi;
Msifuni kwa matari na kucheza;
Msifuni kwa zeze na filimbi;
(K) Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana.

Msifuni kwa matoazi yaliayo;
Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Aleluya.
(K) Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana.

Injili

Lk 6:27-38

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang'anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.

Maoni


Ingia utoe maoni