Masomo ya Misa
Dominika ya 23 ya Mwaka (Jumapili, Septemba 08, 2019)
Hek 9:13-19
Ni mtu yupi awezaye kulijua shauri la Mungu? Au ni nani atakayeelewa na mapenzi yake? Kwa kuwa mawazo ya wanadamu yana woga, na makusudi yetu yanaelekea kushindwa; na mwili wenye uharibifuhuigandamiza roho, na kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbuko. Kwa shida tu twayapambanua yaliyoko duniani, na yaliyo karibu nasi ni kazi kuyaona; lakini yaliyoko mbinguni ni nani aliyeyagundua? Naye ni yupi aliyeyavumbua mashauri yako, isipokuwa ulimpa Hekima na kumpelekea Roho yako takatifu kutoka juu? Ndivyo mienendo yao wakaao duniani ilivyosafishwa, na wanadamu walivyofundishwa yakupendezayo; hata na kwa Hekima wao wenyewe waliponywa.
Zab 90:3-6, 12-14, 17
Wamrudisha mtu mavumbini,
usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi.
Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi.
Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi.
Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu uithibitishe.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi.
Flm 1:9c-10, 12-17
Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.
Efe 1:17, 18
Aleluya, aleluya
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Uyatie nuru macho ya mioyo yetu, Ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya
Lk 14:25-33
Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Maoni
Ingia utoe maoni