Masomo ya Misa
Ijumaa ya 17 ya Mwaka (Ijumaa, Agosti 02, 2019)
Law 23:1,4-11, 15-16,27, 34-37
Bwana akanena na Musa, na kumwambia: Sikukuu za Bwana ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya Bwana. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa Bwana ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba. Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi. Lakini mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyikko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi. Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu; naye atautikisa mganda mbele za Bwana ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya sabato kuhani atautikisa. Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia sabato saba; hata siku ya pili ya hiyo sabatos ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka ya unga mpya. Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa Bwana. Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi. Mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yoyote ya utumishi. Sikukuu za Bwana ni hizi, ambazo mtazipigia mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee Bwana sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake.
Zab 8:2-5, 9-10
Pazeni zaburi, pigeni matari,
Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda.
Pigeni panda mwandamo wa mwezi,
Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu.
(K) Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha.
Kwa maana ni sheria kwa Israeli,
Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo.
Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu,
Alipoondoka juu ya nchi ya Misri;
Maneno yake nisiyemjua naliyasikia.
(K) Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha.
Usiwe na mungu mgeni ndani yako;
Wala usimsujudie mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri;
Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.
(K) Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha.
1The 2:13
Aleluya, aleluya,
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu.
Aleluya.
Mt 13:54-58
Yesu alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.
Maoni
Ingia utoe maoni