Masomo ya Misa
Jumatano ya 16 ya Mwaka (Jumatano, Julai 24, 2019)
Kut 16:1-5, 9-15
Walisafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli. Njoni karibu mbele ya Bwana; kwa kuwa yeye ameyasikia manung’uniko yetu. Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa Bwna ukaonekana katika hilo wingu. Bwana akasema na Musa, akinena, Nimeyasikia manung’uniko ya wana wa Israeli; haya! Sema nao, ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. Ikawa wakati wa jioni; kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle.
Zab 78:18-19, 23-28
Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao
Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao.
Naam, walimwambia Mungu, wakasema,
Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani?
(K) Bwana aliwapa nafaka ya mbinguni.
Lakini aliyaamuru mawingu juu;
Akaifungua milango ya mbinguni;
Akawanyeshea mana ili wale;
Akawapa nafaka ya mbinguni.
(K) Bwana aliwapa nafaka ya mbinguni.
Mwanadamu akala chakula cha mashujaa;
Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.
Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni;
Akaiongoza kusi kwa uweza wake.
(K) Bwana aliwapa nafaka ya mbinguni.
Akawanyeshea nyama kama mavumbi,
Na ndege wenye mbawa,
Kama mchanga wa bahari.
Akawaangusha kati ya matuo yao,
Pande zote za maskani zao.
(K) Bwana aliwapa nafaka ya mbinguni.
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Mbegu ni neno la Mungu, anayepanda ni Kristu, atakayemkuta, ataishi milele.
Aleluya.
Mt 13:1–9
Yesu alitoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye masikio na asikie.
Maoni
Ingia utoe maoni