Masomo ya Misa
Alhamisi ya 12 ya Mwaka (Alhamisi, Juni 27, 2019)
Mwa 16:1-12, 15-16
Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, Bwana amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. Bwana na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa Bwana akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa Bwana akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa Bwana akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa Bwana akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana Bwana amesikia kilio cha mateso yako. Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote.Hajiri akamzalia Abramu mwana wa kiume; Abramu akamwita jina lake Ishmaeli, yule mwanawe, ambaye Hajiri alimzaa. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka themanini na sita, hapo Hajiri alipomzalia Abramu Ishmaeli.
Zab 106:1-5
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana,
Kuzihubiri sifa zake zote?
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
Heri washikao hukumu,
Na kutenda haki sikuzote.
Ee Bwana, unikumbuke mimi,
Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
Unijilie kwa wokovu wako,
Ili niuone wema wa wateule wako.
Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako,
Na kujisifu pamoja na watu wako.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
Mt 7:21-29
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa. Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.
Maoni
Ingia utoe maoni