Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 8 ya Mwaka (Ijumaa, Mei 27, 2016)  

Somo la 1

1Pet 4:7-13

Mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala. Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung'unika; kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina. Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.

Wimbo wa Katikati

Zab 96:10-13

Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki; Naam,
ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili.
(K)Bwana anakuja aihukumu nchi.

Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
(K)Bwana anakuja aihukumu nchi.

Mbele za Bwana, kwa maana anakuja, Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa uaminifu wake.
(K)Bwana anakuja aihukumu nchi.

Shangilio

Yn 15:16

Aleluya, Aleluya
Naliwachagua ninyi kutoka ulimwenguni mkazae matunda yatakayodumu, asema Bwana.
Aleluya

Injili

Mk 11:11-26

Yesu aliingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara. Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.

Maoni


Ingia utoe maoni