Masomo ya Misa
Ijumaa ya 11 ya Mwaka (Ijumaa, Juni 21, 2019)
2Kor 11:18, 21-30
Wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili, mimi nami nitajisifu. Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Walakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri. Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Ibrahimu? Na mimi pia. Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe? Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.
Zab 34:1-6
Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Wenye haki Bwana anawaponya na taabu zao zote.
Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote.
(K) Wenye haki Bwana anawaponya na taabu zao zote.
Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.
(K) Wenye haki Bwana anawaponya na taabu zao zote.
Mt 6:19-23
Yesu aliwaambia wanafunzi: Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!
Maoni
Ingia utoe maoni