Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 8 ya Mwaka (Alhamisi, Mei 26, 2016)  

Somo la 1

1Pet 2:2-5, 9-12

Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili. Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema. Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.

Wimbo wa Katikati

Zab 100:2-5

Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba;
(K) Njoni mbele za Bwana kwa kuimba kwa furaha

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
(K) Njoni mbele za Bwana kwa kuimba kwa furaha

Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake;
(K) Njoni mbele za Bwana kwa kuimba kwa furaha

Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi.
(K) Njoni mbele za Bwana kwa kuimba kwa furaha

Shangilio

Yn 8:12

Aleluya, Aleluya
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya

Injili

Mk 10: 46-52

Walifika Yeriko; Yesu alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.

Maoni


Ingia utoe maoni