Masomo ya Misa
Jumatano ya 7 ya Pasaka (Jumatano, Juni 05, 2019)
Mdo 20:28-38
Paulo aliwaambia wakuu wa kanisa la Efeso: Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.
Zab 68: 28-29, 32-35
Ee Mungu, uziamuru nguvu zako;
Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.
Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu Wafalme watakuletea hedaya.
(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.
Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu,
Msifuni Bwana kwa nyimbo.
Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele;
Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.
Mhesabieni Mungu nguvu;
(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.
Enzi yake i juu ya Israeli;
Na nguvu zake zi mawinguni.
Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako.
Ndiye Mungu wa Israeli;
Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo.
Na ahimidiwe Mungu.
(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.
Yn 17:11-19
Siku ile Yesu alisali akisema: Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.
Maoni
Ingia utoe maoni