Masomo ya Misa
Jumanne ya 8 ya Mwaka (Jumanne, Mei 24, 2016)
1Pet 1:10-16
Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia. Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
Zab 98:1-4
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokuvu wake.
Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Bwana ameufunua wokuvu wake.
Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti,
imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Bwana ameufunua wokuvu wake.
Mt 11:25
Aleluya, aleluya
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya
Mk 10:28-31
Petro alimwambia Yesu, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza.
Maoni
Ingia utoe maoni