Masomo ya Misa
Jumatatu ya 4 ya Pasaka (Jumatatu, Mei 13, 2019)
Mdo 11:1-18
Siku zile, mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wan chi wenye miguu mine, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishwi. Ndugu hawa sita nao wakaenda nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukuia kama alivyotushukia sisi mwanzo. Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohane alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatiza kwa Roho Mtakatifu. Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu? Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba lilitalo uzima.
Zab. 42:1-2, 43:2-3
Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji,
Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, ee Mungu.
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.
Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
Lini nitakapoikuja nionekane mbele za Mungu?
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.
Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako.
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.
Hivyo nitakwenda madhabahuni mwa Mungu,
Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu;
Nitakusifu kwa kinubi, ee Mungu, Mungu wangu.
(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.
Ufu. 1:5
Aleluya, aleluya,
Ee Kristo, yu shahidi aliye mwaminifu mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia.
Aleluya.
Yn. 10:1-10
Yesu aliwaambia Wayahudi: Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang’anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo wake wote, huwatangulia; na awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. Mithali hiyo Yesu aliwaambia; lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.
Maoni
Ingia utoe maoni