Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 7 ya Mwaka (Jumamosi, Mei 21, 2016)  

Somo la 1

Yak 5:13-20

Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake. Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi.

Wimbo wa Katikati

Zab 141: 1-3, 8


Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo.
Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.
(K)Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba

Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.
Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu.
(K)Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba

Shangilio

Mt 11:25

Aleluya, Aleluya
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya

Injili

Mk 10:13-16

Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.

Maoni


Ingia utoe maoni